NEWS

Punguza Maumivu Ya Hedhi Kwa Kula Aina Hii Ya Vyakula

Kuna baadhi ya wanawake ambao hupata maumivu tofauti wakati wa siku za hedhi kila mwezi. Maumivu haya makali na mateso huvuruga ratiba zao za kazi, kulea familia na hata kuacha kufanya shughuli za kujiingizia kipato. 
Wengi hutumia dawa na kupata nafuu, wengine hawapendi dawa maana huleta madhara yasiyotegemewa mwilini na kulazimika kuvumilia mateso hadi yanapoisha baada ya hedhi. Leo katika makala yetu tunaangalia jinsi ya kupunguza maumivu ya hedhi kwa kuangalia vyakula vinavyoweza kutumika kama dawa.

Vyakula ni njia mbadala sababu hutumika kupunguza kiwango cha homoni au kemikali zinazosababisha kuleta maumivu mwilini. Ili kuwa na uelewa mzuri, tuangalie kiini cha tatizo hadi kusababisha maumivu makali wakati wa hedhi, halafu tuangalie vyakula vinavyoweza kutatua tatizo.
CHANZO CHA TATIZOKemikali aina ya prostagland­ins ndio chanzo cha maumivu wakati wa hedhi kwa wanawake. Kemikali hii hutengenezwa na chem­bechembe za mafuta yapatika­nayo kwenye seli. Kazi ya kemikali hii ni kusababisha uvimbe, kusinyaa kwa misuli, kusinyaa kwa mishipa ya damu na kuganda kwa damu.
Muda mfupi kabla ya kuanza hedhi, ukuta wa seli zinazotengeneza prostaglandins hujijenga kwenye mji wa mimba. Wakati wa hedhi, seli hizi hubomoka na kusababi­sha prostaglandis kutoka kwa wingi. Hii husababisha mishipa ya damu kusinyaa, misuli kubana na kusababisha maumivu makali.

Kemikali za prostaglandins huingia pia kwenye mfumo wa damu na kusababisha maumivu ya kichwa, kizunguzungu, kichefuchefu, kutapika na kuharisha. Kiwango cha prostaglandins ni kikubwa sana kwa wanawake wanaopata maumivu wakati wa hedhi kuliko wale wasiopata maumivu.Wanawake wengi wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango hupunguza pia maumivu ya hedhi sababu vidonge huzuia ukuaji wa seli zinazozalisha prostaglandins. Lakini inawezekana pia kufikia malengo kwa kuangalia aina za vyakula.
VYAKULA VIPUNGUZAVYO MAUMIVUVyakula vinaweza kufanya kazi ya kupunguza mauvimu ya hedhi kwa kurekebisha kiwango cha homoni ya oestrogen mwilini.Oestrogen ni homoni ya kike inayotolewa mwilini kwa shughuli za kuzalisha seli. Oestrogen hutolewa kwa viwango tofauti kutegemeana na muda wa mzunguko wa mwanamke huzalishwa kwa wingi sana baada ya hedhi na muda mfupi kabla ya hedhi kuanza.

Ili kuweza kupunguza maumivu, ni vizuri kuzingatia: Punguza vyakula vyenye mafuta. Vyakula vya mafuta  husababisha oestrogen izalishwe kwa wingi, hivyo kuzalisha seli nyingi zaidi kwenye mji wa mimba.
Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber). Nyuzinyuzi husaidia kusafisha mwili kwa kuondoa oestrogen kirahisi toka mwilini, hivyo kupunguza kiwango chake kwenye damu na kuzuia kukua kwa seli kwenye mji wa uzazi. Kula nafaka, mboga za majani na matunda kwa wingi. Jamii hii ya vyakula ina nyuzinyuzi (fiber) inayotumika katika kupunguza kiwango cha oestrogen mwilini pia kunywa juisi za matunda halisi.
Acha kunywa pombe au kula vyakula vya kusindika, visivyo asili maana huwa na mafuta mengi yanayoweza kukusababisha matatizo zaidi. Kubadilisha vyakula inasaidia sana. Wanawake wengi hufurahia matokeo na hata kuwaza kwa nini wasingefanya hili zoezi mapema.Kula chakula bora na kupunguza uzito wa mwili ili uwe na afya bora. Ni muhimu kuzingatia kula vyakula vya jamii ya nafaka, mboga za majani na matunda.